ZITTO KABWE AIBUKA NA DVD MATATA SANA, SOMA UJUE INAHUSU NN
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
WAKATI Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe,
akijipanga kuanza ziara katika mikoa kadhaa nchini kujibu mapigo ya
tuhuma dhidi yake zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenye ziara ya
Operesheni M4C Pamoja
Daima, mbunge huyo ameibuka na DVD inayowananga viongozi wa CHADEMA.
Vyanzo vyetu vya habari vilisema kuwa DVD hizo zitasambazwa kwenye
mikoa na maeneo yote atakayofanya mikutano ya hadhara mbunge huyo, kama
moja ya harakati na mikakati ya kujisafisha na tuhuma za usaliti
zinazomkabili ndani ya chama.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa DVD hizo
zinatengenezwa kwenye kampuni moja iliyopo eneo la Kariakoo ambayo
imepewa tenda ya kuchapa nakala 10,000 na kampuni nyingine zaidi ya
tatu, nazo zimepewa tenda ya kuchapa DVD hizo kwa idadi tofauti.
Hata hivyo jambo la kushangaza ni kwamba katika jaradio la DVD hizo
kuna rangi ya njano, nyeupe, bluu nyepesi, bluu nzito pamoja na bendera
ya taifa.
Rangi zilizotumika kwenye jaradio hilo hazina uhusiano na rangi za bendera ya CHADEMA wala chama chochote cha siasa nchini.
Mbali ya jaradio hilo kupambwa na rangi hizo, pia limepambwa na picha
kadhaa za mikutano aliyopata kuifanya mwanasiasa huyo katika maeneo
mbalimbali na nyakati tofauti nchini, huku picha kubwa ikimwonyesha
Zitto akiwa amevalia suti huku akitabasamu.
Jaradio hilo pia limezungukwa na maandishi mbalimbali ambayo yanasomeka:
‘Uadilifu,
Uzalendo na Uwajibikaji, ndio silaha yetu katika kutetea wanyonge na
maskini wote wa Tanzania, tuungane kwa pamoja.’ ‘Tanzania Kwanza’
Maandishi mengine makubwa yanamtambulisha mbunge huyo ambayo nayo yanasomeka:
‘Zitto Zuberi Kabwe, Mtetezi wa Wanyonge, Tumaini la Maskini wa Tanzania”
Jaradio hilo pia limeweka mawasiliano ya mbunge huyo ya simu ya mkononi, barua pepe, Facebook na Twitter.
Hakuna maelezo yanayoonyesha kama DVD hizo zinauzwa au zinatolewa bure.
Ndani ya DVD
DVD hizo ambazo nakala tunayo, zinaonyesha picha ya mikutano ya
hadhara ya mbunge huyo aliyoifanya mkoani Kigoma mara baada ya Kamati
Kuu (CC) ya CHADEMA kumvua nyadhifa zake na Mahakama Kuu kushikilia
hatima ya uanachama wake baada ya kukabiliwa na tishio la kuvuliwa
uanachama.
Kwa mujibu wa DVD hizo, katika moja ya mikutano ya
mkoani Kigoma, Zitto anasikika akiuambia umati wa wafuasi wake
waliofurika kumsikiliza akieleza chanzo cha mgogoro wake na CHADEMA ni
msimamo wake wa kuhoji hesabu za fedha za vyama vya siasa, kikiwemo
CHADEMA na kumuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), kufanya uhakiki.
Kama ambavyo amepata kukaririwa mara kwa
mara, Zitto ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC) anasema CHADEMA ilimtaka awajulishe kwanza kabla ya
kumuagiza CAG kufanya ukaguzi ili kutoa fursa ya kuweka hesabu zao
vizuri.
DVD hiyo pia inamuonyesha Zitto akisema sababu nyingine
ya ugomvi wake na CHADEMA ni dhamira yake ya kutaka kuwania uenyekiti wa
CHADEMA, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Freeman Mbowe, Mbunge
wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Huku
akishangiliwa na maelfu ya wafuasi wake, baadhi wakiwa na mabango ya
kumsifia, Zitto anasema hajawahi kupewa fedha na CCM kuisaliti CHADEMA
na kuongeza kwamba atakuwa wa mwisho kutoka ndani ya chama hicho
alichojiunga nacho akiwa na umri wa miaka 16.
Dk. Kitila Mkumbo naye yumo
DVD
hiyo pia inamuonyesha aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Baraza Kuu la
CHADEMA, Dk. Kitila Mkumbo, akieleza sababu za yeye kutaka kujiuzulu
kabla ya Kamati Kuu kuamua kumvua uanachama.
Dk. Kitila pia
anaonekana kwenye DVD hiyo akielezea waraka ulioandikwa na Samson
Mwigamba ambao ulinaswa ukielezea mikakati ya kutaka kuung’oa uongozi wa
Mbowe kwenye nafasi ya uenyekiti.
Kwa kifupi maelezo ya Dk.
Kitila ni yale aliyopata kuyatoa siku yeye na Zitto walipofanya mkutano
na vyombo vya habari katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam
wakitetea waraka huo kwamba haukuwa wa uasi kama ilivyotafsiriwa na
CHADEMA.
Wiki iliyopita gazeti hili liliibua mkakati unaodaiwa
kufadhiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kutaka kumtumia Zitto
kupambana na CHADEMA waziwazi.
Katika mkakati huo CCM inadaiwa
kutaka kukodisha helikopta ya kumpeleka Zitto katika mikoa minne kwa
gharama ya sh milioni 50, mara tu baada ya CHADEMA kuhitimisha
Operesheni yao ya M4C Pamoja Daima.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka
vyanzo vilivyo karibu na Zitto na CCM, yeye na chama hicho sasa wana
adui mmoja – CHADEMA; na wameamua kujibu mapigo baada ya kuridhika
kwamba kwa vyovyote Zitto amekwisha kupoteza uanachama wake katika
CHADEMA.
Nia yao ni kumtumia Zitto kuleta mpasuko katika CHADEMA,
na kufunika mjadala wa mgogoro wa CCM, kero za wananchi na mchakato wa
Katiba mpya.
Zitto ambaye alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya
CHADEMA – Naibu Katibu Mkuu Bara, Mjumbe wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Baraza
Kuu na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni – anatarajia
kutumia helikopta yenye uwezo wa kubeba watu wanne, ambayo inadaiwa
kukodishwa na wapinzani wa CHADEMA.
Kwa mujibu wa habari hizo,
lengo la ziara ya Zitto ni kujibu mapigo ya CHADEMA, hasa katika maeneo
ambayo baadhi ya makada na viongozi wa chama hicho wamepita na
kuzungumzia hatima yake kisiasa, hasa walipojibu maswali ya wananchi
kuhusu sakata lake kuvuliwa uongozi kwa tuhuma za usaliti, na hatimaye
Zitto kwenda mahakamani kuzuia chama kujadili uanachama wake.
Katika
kesi ya msingi, Zitto aliyewahi kuwa maarufu akiwa kiongozi wa CHADEMA,
anaomba arudishiwe nyadhifa zake zote, na apatiwe nakala za uamuzi wa
Kamati Kuu (CC) ili aweze kukata rufaa Baraza Kuu.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA
0 comments: